"Tuma kwa Namba Hii" MIKONONI MWA POLISI
Na Paschal D.Lucas,(Geita)
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kukutwa na laini za simu 9,389 za mitandao mbalimbali ya simu, ambazo walikuwa wakizitumia kufanyia uhalifu kwa njia ya mtandao na unyang'anyi.
Watuhumiwa hao pia wamekutwa na vifaa mbalimbali vya kufanyia uhalifu ikiwemo kompyuta mpakato, mashine mbili za kusajili laini kwa kutumia alama za vidole, simu janja 15 na simu ndogo za kawaida 18.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Safia Jongo imeeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa Machi 13, 2025 katika Kata ya Ludete wilayani Geita ambapo Jeshi la Polisi lilipata taarifa juu ya uwepo wa wahalifu hao na kuweka mtego uliofanikisha kuwakamata wakiwa na vifaa vya kufanyia uhalifu.
Jeshi la Polisi mkoani Geita linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kuweza kubaini mtandao mzima wa wahalifu hao na kuwachukulia hatua za kisheria.

Comments
Post a Comment