ALICHOKISEMA WAZIRI MKUU KWENYE JUBILEI YA MIAKA 25 YA UASKOFU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema jamii inahitaji kufundishwa, kutambua na kuenzi mila za Kitanzania na kuepuka kuiga tabia za kigeni zisizo na manufaa kwa ustawi wa Taifa.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo, Machi 19, 2025, wakati wa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Bukoba, Askofu Method Kilaini.
"Tumeshuhudia ongezeko la vitendo vya ukosefu wa maadili katika jamii. Hali hii inatokana na malezi hafifu na kuiga mila na desturi kutoka mataifa mengine ambazo haziendani na tamaduni na maadili yetu ya Kitanzania," amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa mabadiliko haya yameathiri hasa vijana, yakiyumbisha misingi ya familia na jamii kwa ujumla. Ameomba Kanisa kuendelea kuwa nguzo ya maadili bora, likitoa mwongozo wa kiroho na kijamii.
Pia, ameeleza kutambua mchango wa madhehebu ya dini, ikiwemo Kanisa Katoliki, katika kuboresha ustawi wa jamii na kuahidi ushirikiano wa Serikali katika kulinda na kuimarisha maadili ya Kitanzania kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Comments
Post a Comment